25 Aprili 2016 - 17:58
Obama : Ulaya madhubuti muhimu kwa maendeleo ya dunia

Rais Barack Obama wa Marekani amesema Marekani inahitaji kuwa na Ulaya madhubuti ilioungana ili kudumisha utulivu wa kimataifa na kuhimiza kile alicho kidai kuwa kuongeza matumizi ya ulinzi kupambana na kundi la kigaidi la Daesh.

Shirika la habari la ABNA linaripoti kuwa: Rais Barack Obama wa Marekani amesema Marekani inahitaji kuwa na Ulaya madhubuti ilioungana ili kudumisha utulivu wa kimataifa na kuhimiza kile alicho kidai kuwa kuongeza matumizi ya ulinzi kupambana na kundi la kigaidi la Daesh.

Akikamilisha ziara yake nchini Ujerumani ambayo ilikuwa imelenga kuimarisha uhusiano wa kibiashara Obama amewasihi viongozi wa Ulaya kuangalia kupindukia matatizo lukuki yanayayakabili mataifa yao na kudumisha umoja ambao umeleta amani katika bara lao.

Kauli yake hio inakuja baada ya ziara yake aliyofanya awali huko London ambapo aliihimiza Uingereza kuendelea kubakia katika Umoja wa Ulaya wenye nchi wanachama 28 na hiyo kuimarisha juhudi za Waziri Mkuu David Cameron kuepuka kile kinachoitwa "Brexit" yaani kujitowa kwa Uingereza katika umoja huo ambao wanaopinga wanasema kunaweza kuchochea madhara ya kisiasa na kiuchumi kwa nchi hiyo.

Akizungumza wakati akiyatembelea maonyesho ya biashara na viwanda mjini Hannover Jumatatu Obama amesema amekuja kuwakumbusha watu wa Ulaya mafanikio makubwa kabisa waliyoyapata wakiwa kama Umoja wa Ulaya.

Ulaya madhubuti muhimu kwa dunia

"Umoja wa Ulaya ulio madhubuti ni muhimu kwa dunia kwa sababu Ulaya ilioungana inabakia kuwa muhimu kwa ututulivu wetu wa kimataifa. Ulaya inasaidia kudumishwa kwa kanuni na sheria ambazo zinaweza kudumisha amani na kukuza ustawi duniani kote."

Obama amesema wasi wasi kuhusiana na kunyakuliwa kwa Crimea kulikofanywa na Urusi na kuzorota kwa ukuaji wa uchumi hususan kusini mwa Ulaya kumepelekea kuzuka kwa mashaka kuhusu kuungana kwa bara hilo na kuchochea siasa haribifu ambazo nazo zimepalilia hofu kuhusu wahamiaji na watu wenye dini tafauti.

Wimbi la wahamiaji wanaokimbia vita nchini Syria limeongeza mvutano katika Umoja wa Ulaya na kuweka shinikizo kwa Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ambaye anaonekana kuwa kiongozi mwenye sauti barani Ulaya na ambaye sera yake ya awali ya kufunguwa milango imeathiri msimamo wake wa kisiasa ndani ya nchi.

Ishara kumuunga mkono Merkel

Ziara hiyo ya siku mbili ya Obama nchini Ujerumani inaonekana kuwa ni ishara ya kumuunga mkono kiongozi huyo ambaye wamejenga uhusinao wa karibu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Ujerumani mwakani.

Ziara hiyo pia imeoyesha kumuunga mkono Merkel na Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameroon kwa dhana pana zaidi ya dhima ya Umoja wa Ulaya kwa dunia.

Obama amesema huu ni wakati muhimu sana na kile kinachotokea katika bara hili kitakuwa na taathira zake kwa watu duniani kote.

Obama atembelea maonyesho ya biashara Hannover

Rais Barack Obama ametembelea maonyesho ya biashara na viwanda ya Hannover pamoja na Kansela Angela Merkel kabla ya kuwa na mazungumzo na viongozi wa Ulaya juu ya masuala ya dunia na usalama.

Akizungumza akiwa katika banda la Marekani Rais Obama amesema "kiasi kikubwa sana cha uchumi wetu wa dunia na ukuaji unaozalisha nafasi za ajira unachochewa na mwamko wa ubinifu, ugunduzi, kutunga na baadae kuzigeuza fikra hizo kuwa bidhaa mpya, kuwa kampuni kuwa viwanda vipya na huduma mpya mambo ambayo huzalisha ajira nzuri."

Amesema hiyo hii ni fursa nyengine kwake kumwambia kila mtu aje hapo na kununuwa bidhaa zilizotengenezwa Marekani.

Rais Barack Obama wa Marekani akizungumza akiwa katika banda la Marekani leo hii wakati alipotembelea maonyesho hayo ya biashara na viwanda ya Hannover akiandamana na mwenyeji wake Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ambapo amesema yuko Hannover kwa sababu ana fahari kuonyesha mwamko wa ubunifu wa Marekani.

Kufunguliwa rasmi kwa maonyesho

Merkel na Obama walifunguwa rasmi maonyesho hayo ya makubwa kabisa ya biashara na viwanda duniani ya Hannover Messe hapo jana.Marekani kwa mara ya kwanza imekuwa nchi mshirika katika maonyesho hayo

Wakati wakianza kukaguwa mabanda ya Marekani na Ujerumani katika maonyesho hayo Kansela Angela Merkel wa Ujerumani alitamka kwa Kingereza kwa kuwa utamu wa puding ni kuila basi na waanze.

Obama na Merkel walitembelea vibanda vya Marekani vya kutengeneza mashine za kuchapisha za 3D ,vifaa vya kompyuta na teknolojia ya anga za juu wakiandamana na mkururo wa wapiga picha, waandishi wa habari, maafisa usalama na mawaziri.

Marekani kupeleka wanajeshi 250 Syria kwa madai ya kupambana na Daesh

Rais Obama pia ametangaza uwekaji wa wanajeshi wa Marekani 250 nchini Syria wengi wakiwa katika kikosi cha operesheni maalum kwa kile alichodai kuwa ni kupambana na magaidi wa Daesh.

Jioni hii Obama anaungana na Merkel kwa mazungumzo juu ya masuala yanayoikabili dunia hivi sasa ambayo pia yatahudhuriwa na Rais Francois Hollande wa Ufaransa, Waziri Mkuu wa Italia Matteo Renzi na Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron.

Mazungumzo hayo ambayo yanatajwa kwa mkutano mdogo wa kilele pia yatagusia mapambano dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh nchini Syria na Iraq,mzozo wa wakimbizi barani Ulaya ,mzozo wa Libya, kura ya maoni ya Uingereza juu ya uwanachama wake wa Umoja wa Ulaya na makubaliano ya biashara kati ya Marekani na Ulaya yanayopendekezwa pamoja na hatua za kudhibiti mabavu ya Urusi.

Marekani imekuwa ikiyasaidia makundi ya kigaidi nchini Syria kwa lengo la kuiangusha serikali ya Syria lakini haikuweza kufanikiwa kutokana na Majeshi ya Iran na Urusi kuingilia kati na kupambana na magaidi hao hatari wanaotumwa na Marekani na washirika wake.

Mwisho wa habari/ 291